Tanzania na Rwanda zapiga hatua nyingine
katika ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) yenye urefu wa km521 kutoka Isaka hadi
Kigali baada ya mawaziri wa uchukuzi wa chi hizo mbili kukutana siku ya tarehe
20 January 2018 jijini Dar es Salaam kujadili namna ya kutekeleza mradi huo
kufuatia agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe
Magufuli la kukutana kwa mawaziri hao wawili mapema.
Katika mkutano huo waziri wa Ujenzi, Uchukuzi
na Mawasiliano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Prof. Makame Mbarawa na
waziri wa Miundombinu wa Jamhuri ya Rwanda Mhe. James Musoni walijadili na
kutoa mapendekezo ya namna ya utekelezaji wa mradi huo.
Mkutano huo uliofanyika jijini Dar es Salaam
kwenye ofisi za Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ulihudhuriwa pia na
mawaziri kutoka Tanzania akiwemo Waziri ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Africa Mashariki Mhe. Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Mipango na Fedha, Dkt.
Philip Mpango, Balozi wa Jamhuri ya Rwanda nchini Tanzania Mhe. Eugene
Kayihura, makatibu wakuu wa Wizara za uchukuzi wa nchi za Rwanda na Tanzania pamoja
na maafisa waandamizi wengine kutoka nchi hizo mbili.
Mawaziri wa nchi hizo mbili wameeleza kuwa
wamejitoa kuhakikisha ushirikiano na mahusiano ya kibiashara katika nchi hizo
mbili unakua, lengo likiwa ni kukuza uchumi na kuziletea maendeleo nchi hizo
mbili, kwakuwa kukamilika kwa ujenzi wa reli hiyo ya Isaka-Kigali kunatarajiwa
kupunguza gharama za usafirishaji wa mizigo na kuongeza kiasi cha mizigo
inayosafirishwa kwenda nchini Rwanda kupitia Bandari ya Dar es Salaa.
Mawaziri hao wawili wamekubaliana kutumia
upembuzi uliofanywa katika nchi hizo mbili katika kipindi kilichopita kujenga
reli inayofanana na inayojengwa kutoka Dar-Morogoro hadi Makutupora kwa lengo
la kuwa na viwango stahiki vinavyofanana.
Makubaliano ya ushirikiano wa pamoja
yalisainiwa na Waziri wa Miundombinu wa Rwanda Mhe. James Musoni na Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano wa Tanzania Prof. Makame Mbarawa, makubaliano
yaliyolenga kuunganisha nguvu katika ujenzi wa reli hiyo ambapo kila nchi
itagharamia ujenzi wa reli hiyo ya kisasa katika eneo lake.
No comments:
Post a Comment