IFAHAMU HISTORIA YA KICHWA CHA TRENI KINACHOTUMIA INJINI YA MVUKE KILICHOBAKIA TANZANIA - TRC Blog

Home Top Ad

"TOGETHER WE MOVE"

Tuesday, October 24, 2017

IFAHAMU HISTORIA YA KICHWA CHA TRENI KINACHOTUMIA INJINI YA MVUKE KILICHOBAKIA TANZANIA

Injini ya mvuke ni injini inayotumia nguvu ya mvuke kwa kufanya kazi, nguvu ya mvuke ni nishati ya joto iliyomo ndani yake, nishati hii inabadilishwa kuwa mwendo. Ndani ya mashine maji hupashwa moto na kugeuka kuwa mvuke, mvuke huingia katika silinda ambako husukuma pistoni ndani yake. Mwendo wa pistoni unabadilishwa kuwa mwendo wa kuzunguka kupitia fitokombo.
Injini za kwanza za mvuke zilitengenezwa kwa ajili ya kuendesha pampu za kuvuta maji kwenye migodi ya makaa huko Uingereza. Kuanzia miaka ya 1780 mafundi waliongeza gia na fitokombo na hivyo injini ya mvuke ilitumiwa hata viwandani kuendesha mashine mbalimbali zilizowahi kutumia awali nguvu ya wanadamu au ya wanyama. Mhandisi James Watt anakumbukwa kwa uboreshaji wa injini za kwanza.
Injini za mvuke ziliendelea kusukuma magari ya kwanza barabarani au kwenye reli. Jina la "gari la moshi" bado linakumbuka asili hii, japokuwa hivi leo injini za dizeli au umeme si mvuke tena. Siku hizi injini za mvuke karibu zimepotea kiwandani na pia kwenye magari.
Bado kuna matumizi ya aina ya injini ya mvuke katika vituo vya umeme, japo aina hii ya injini ni chache katika ulimwengu huu wa matumizi ya mafuta na nishati nyingine mbadala. Kwa hapa Tanzania tulibahatika kupata nafasi ya kuwa na injini za mvuke zilizokuwa kwenye vichwa vya treni zilizokuwa zikibeba abiria na mizigo tangu mwaka 1954 lilipokuwa shirika la reli la Afrika Mashariki ‘East African Railways’ ambapo vilikuwepo vichwa zaidi ya arobaini (40) vilivyokuwa vinavyotumia injini ya mvuke kufanya shughuli za usafiri Afrika Mashariki.
Muonekano wa Mbele wa Kichwa cha treni kilichokuwa kikitumia injini ya mvuke
Hapa Tanzania katika Kampuni ya Reli (TRL) kumekuwapo na kichwa cha treni kimoja ambacho kilikuwa kikitumia ‘Injini ya Mvuke’, japokuwa kulikuwako na vichwa kadhaa miaka ya 1960 hadi 1990 ambavyo vilikuwa vikitumia injini hiyo ya mvuke. Kichwa hicho cha treni kilichopewa jina la ‘SUK’ 2927XX kiliundwa mnamo mwaka 1955 na kampuni ya NORTH BRITISH LOCOMOTIVE GLASSGLOW LIMITED ya huko nchini Uingereza. Imeelezwa kwamba jina hilo lilitokana na kabila moja la waganda ambalo linapatikana huko nchini Uganda. Injini hii ya treni aina ya SUK ilianza shughuli zake mnamo mwaka 1954 ikifanya shughuli kuu ya kusafirisha abiria na mizigo kati ya Tanga na Moshi.
Muonekano wa Kichwa cha treni aina ya SUK kilichokuwa kikitumia injini ya mvuke 
Kichwa hiki cha treni kilikuwa na uwezo wa kubeba tani 750 hadi 800 za mizigo na abiria na ilikua na uwezo wa kufanya kazi kama treni inayotumia mafuta ya dizeli. 
Kichwa hicho cha treni kilifanya kazi kwa takribani miaka thelathini (30) kuanzia mwaka 1954-1984, treni hiyo haikuweza tena kuendelea kutembea kutokana na kuanza kutumika kwa injini za mafuta ya Dizeli ambazo zilianza kutumika miaka ya 1977 baada ya kufa East Africa Railways na kuanzishwa Shirika la Reli la Tanzania (TRC1) mnamo mwaka 1977.
Ilipofika mwaka 1998 Mzungu aliyefahamika kwa jina la Mike Dean kutoka Uingereza alitoa wazo la kuifufua Injini hiyo ya mvuke ili iweze kutumika kwa ajili ya usafiri wa abiria huku lengo lake kubwa likiwa ni kufanya shughuli za kiutalii kupitia kichwa hiko che treni. Mike Dean alishirikiana na Shirika la Reli Tanzania (TRC1) alifanikiwa kukifufua kichwa hicho cha treni na kubadilisha mfumo wa nishati kutoka ule wa awali wa kutumia Maji na Makaa ya Mawe na kuanza kutumia Mafuta mazito (Industrial Oil).
Sehemu ya Injini ambako makaa ya mawe yalikuwa yakiwekwa na kuwashwa moto
Baada ya kukifufua kichwa cha Treni kilifanya kazi kwa muda wa takribani miaka kumi, kuanzia mwaka 1998 hadi mwaka 2007 ambapo kilikuwa kikifanya safari zake kati ya Dar es Salaam na Soga. Wasafiri wake wengi walikuwa ni watalii kutoka nchi za kigeni, huku nauli iliyokuwa ikitozwa  kwa wakati huo kutoka Dar hadi Soga ni Shilingi 10,000 kwa watu wazima na Shilingi 3,000 kwa watoto.
Mike aliendelea kuitangaza treni hiyo kwa wageni kutoka  nje ya Tanzania katika mahoteli waliyokuwa wakifikia, imeelezwa kwamba Mike alikuwa akiitangaza treni hiyo kwa kutumia vipeperushi alivyokuwa akibandika maeneo ya karibu na hoteli hizo na wakati mwingine alikuwa akiwapatia vipeperushi wageni waliokuwa wakija Tanzania kwa shughuli tofauti ikiwemo utalii. Miongoni mwa hoteli kubwa ambazo Mike alikuwa akizitembelea kutangaza utalii wa treni ni pamoja na Kilimanjaro kwa sasa Kempiski, Sheraton kwa sasa Moven pick, Slip way, n.k
Sehemu ambayo ilikuwa ikionesha vipimo vya joto, mvuke na mwendokasi kwenye injini hiyo
Mike alifanikiwa kupata watalii kutoka nchi mbali mbali ikiwemo Brazil, Uingereza n.k, ambapo alikuwa akishirikiana na shirika la reli la wakati huo kuandaa vikundi vya ngoma za kiutamaduni na wasanii wengine wa sanaa kutumbuiza na kuvutia watalii zaidi.
Pamoja na ukuukuu wake, wataalamu wa magari moshi wameeleza kwamba upo uwezekano wa chombo hiko kufanyiwa ukarabati na kuanza kutumika upya kama ambavyo ilifanywa na Mike Deen mnamo mwaka 1998. Kampuni ya Reli lipo kwenye mchakato wa kuangalia uwezekano wa kukifufua tena kichwa hiko ili kiweze kufanya kaz tena. 
Mmoja wa wafanyakazi waliokuwa wakifanya kazi kwenye kichwa cha treni kiitwacho SUK kilichokuwa kikitumia injini ya mvuke, Mzee Hamis Mfaume akitoa maelezo jinsi injini hiyo ilivyokuwa ikifanya kazi

1 comment:

  1. NAIPONGEZA HATUA YA TRL YA KUKIFUFUA KICHWA CHA INGINE HIYO YA ZAMANI [KICHWA GARI MOSHI HILO] KUKIFANYIKA UTAFITI VIZURI KITAFAA KWA KUFANYA UTALII HASA KAMA KITAWEZA KUFANYA SAFARI ZA HADI KUFIKA MIKUMI NATIONAL PACK

    ReplyDelete