Historia ya Reli Tanzania - TRC Blog

Home Top Ad

"TOGETHER WE MOVE"

Historia ya Reli Tanzania

Historia ya reli nchini Tanzania inatajwa kuanza kuwapo visiwani Zanzibar miaka ya 1880 chini ya utawala wa Sultani Bargash ambaye alijenga reli visiwani humo yenye urefu wa Km 10 ikiunganisha Hekalu lake lililokuwa Chukwani kisiwani humo na maeneo ya mjini. 
Reli ya Tanganyika ilianza kujengwa na utawala wa Wajerumani kuanzia Tanga mwaka 1893 na kufika Muheza mwaka 1896, Mombo 1905 na Moshi 1911. Utawala huo ulianzisha kampuni iliyoitwa ‘Germany Colonial Railway Construction and Administration Company’ kwa lengo la kuiendesha reli ya Tanga-Moshi (‘the Usambara Railway’) amabayo ilianza kufanya kazi mwaka 1912. Uamuzi wa kuiendeleza reli hadi Arusha ulifikiwa mwaka 1911 na ujenzi ulikamilika 1929 na reli kufunguliwa mwaka huo huo na Gavana wa wakati huo ‘Sir Donald Cameron’.
Kituo cha treni cha Tanga mwaka 1890. Katika kituo hiki ndiko reli ilikoanza kujengwa mwaka 183.
Upimaji wa Reli ya Kati (‘Central line’) kuunganisha DSM na ziwa Tanganyika ulifanywa mwaka 1894 na ujenzi kuanza mwaka 1905; ikafika Tabora 1912 na Kigoma mwaka 1914.
Mtandao wa Reli kabla na baada ya uhuru wa Tanganyika.
Kituo cha Treni cha Mikese mkoani Morogoro mwaka 1909.
Kituo cha Treni cha Tabora mwaka 1910.
Kituo cha Treni cha Morogoro mwaka 1912.
Kituo cha Treni cha Kidete mkoani Morogoro mwaka 1914.
Vita Kuu ya kwanza dunia iliyoanza 1914 hadi 1918 kati ya Wajerumani na Waingereza ilipelekea Tanganyika kutawaliwa na Waingereza baada ya kuwashinda Wajerumani. Waingereza waliendeleza ujenzi wa reli na mnamo mwaka 1928 reli ilifika Mwanza kutoka Tabora. Reli ya kutoka Kaliua kwenda Mpanda ilikamilika mwaka 1949 na kufunguliwa kwa ajili ya usafirishaji wa mizigo.
Ujenzi wa reli chini ya wakoloni uliendelea hadi mwaka 1960 ambapo reli ya Kilosa kwenda Mikumi ilijengwa. Reli nyingine zilizojengwa kipindi cha ukiloni wa Mwingereza na ile ya kiunganishi cha Kenya na Tanzania, yaan kutoka Voi hadi Kahe mnamo mwaka 1924. Hali kadhalika, mwaka 1932 reli kutoka Manyoni hadi Singida ilijengwa na mnamo 1933 ikafika Kinyangiri eneo lililokuwa mashuhuri kwa uzalishaji wa karanga. Hata hivyo, iling’olewa na baadaye kujengwa upya na Serikali ya Tanzania kuanzia Manyoni mwaka 1985 na kufika Singida mwaka 1997.
Ujenzi wa reli kutoka Msagali hadi Kongwa ulianza mnamo mwaka 1947 na baada ya miaka miwili yaan 1949 reli hiyo ilifika Hogoro (Kongwa) eneo lililokuwa mashuhuri kwa uzalishaji wa karanga. Hata hivyo, reli hii iling’olewa baadaye. Mwaka 1949 hadi 1958 reli ya Nachingwea-Ruo-Chilungula na Masasi mkoani Mtwara ilijengwa, japo ilikuja kung’olewa mwaka 1963.
Mwaka wa 1963, reli kutoka Mruazi hadi Ruvu Junction ilijengwa na serikali ya Tanganyika ili kuunganisha reli ya Tanga na ya reli ya Kati. Huo ndiyo mtiririko wa ujenzi wa reli kuanzia wakoloni hadi baada ya uhuru.
MADHUMUNI YA WAKOLONI KUJENGA RELI
Lengo kuu la Wajerumani kujenga reli lilikuwa kusafirisha mazao ya biashara kama katani, kahawa, pamba, karanga, ngano, mpira n.k. kutoka maeneo ya uzalishaji kwenda kwenye masoko ndani na nje ya nchi, ili kukidhi mahitaji yaliyotokana na mapinduzi ya viwanda (Industrial revolution). Sambamba na hilo walianzisha usafirishaji wa abiria.
Baadhi ya Injini zilizokues zikitumika wakati wa Ukoloni kusafirisha abiria na mizigo.
MUUNDO YA RELI BAADA YA UHURU
Baada ya Tanganyika kupata Uhuru tarehe 9 Desemba, 1961; Serikali mpya iliendelea kutoa huduma ya kusafirisha abiria na mizigo kwa msukumo zaidi. Nchi tatu za Afrika Mashariki Kenya, Uganda na Tanzania ziliungana na kuunda Jumuiya ya Afrika Mashariki (‘East Africa Community’) mwaka 1967 kwa lengo la kuunganisha nguvu katika nyanja za usafirishaji na mawasiliano.
Shirika la Reli na Bandari la Afrika Mashariki (‘East Africa Railways and Harbours’) ni kati ya taasisi zilizoundwa kuwezesha biashara na mawasiliano kati ya nchi hizi tatu na watu wake. Wananchi wa nchi hizi wakawa huru kutembeleana na kufanya biashara kwa kutumia barabara, reli, meli na ndege. Usafiri wa ndege ulikuwa chini ya Shirika la Ndege na mawasiliano yalifanyika kupitia Shirika la Posta la Afrika Mashariki.
Shughuli za Ishara na mawasiliano ya Reli kwa wakati huo zilisimamiwa na kitengo maalum cha Shirika la Posta na Simu la Afrika Mashariki (‘East African Posts and Telecommunication- EAP&T’).
Shirika la Reli na Bandari Afrika Mashariki lilitenganishwa na kuundwa taasisi mbili zinazojitegemea za Shirika la Reli Afrika Mashariki (‘East Africa Railways Corporation’) na Shirika la Bandari Afrika Mashariki (‘East Africa Harbours Corporation’). Shirika la Reli Afrika Mashariki lilianzishwa rasmi tarehe 1 juni, 1969 ambapo madhumuni yake makuu yalikuwa na usafirishaji wa mizigo na abiria kwa nchi wanachamna na nchi jirani (landlocked).
Ili kupata kiunganishi kizuri cha usafiri wa abiria na mizigo kwa nchi jirani, Shirika la Reli lilitumia usafiri wa majini (meli) kupitia maziwa ya Victoria, Nyasa na Tanganyika. Baadhi ya meli zilizotumika ni Mv. Victoria. Ziwa Tanganyika lilikuwa na meli za Mv. Liemba, Mwongozo na Sangara. Ziwa Nyasa lilikuwa na meli za Mv.Iringa na Mv Songea.
Usafririshaji wa mizigo na abiria uliendelea kuwa kazi madhubuti ya Shirika la Reli Afrika Mashariki ambalo lilikuwa na uwezo wa kubeba mizigo mikubwa na mingi kwa wakati mmoja. Mazao yaliyosafirishwa kipind cha Jumuiya ya Afrika Mashariki yaliendelea kuwa yale ya kipindi cha ukoloni, pamoja na kwamba uliongezeka usafirishaji wa bidhaa za viwandani. Jumuia ya Afrika Mashariki ilileta ufanisi mzuri wa usafirishaji wa abiria na mizigo kutoka nchi moja hadi nyingine.
Kituo cha Treni cha Dar es Salaam mwaka 1972