Utangulizi
Shirika
la Reli Tanzania, ni shirika la Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
liloundwa chini ya Sheria ya Reli Namba 10 ya mwaka 2017 ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania kwa lengo kuu la kutoa huduma ya usafiri wa njia ya Reli,
Kusimamia, kuendeleza na kuhakikisha ulinzi na usalama wa miundombinu ya reli
nchini Tanzania.
Historia
Historia
ya Shirika la Reli Tanzania inaweza kuanza kutajwa mnamo mwaka 1948
lilipoanzishwa Shirika la Reli na Bandari za Afrika Mashariki (EAR&H). Shirika
la reli na bandari za Afrika ya Mashariki liliundwa mnamo mwaka 1948
sambamba na Jumuiya ya Afrika Mashariki na lilikuwa Shirika la umma
lililosimamia reli na bandari za Kenya, Uganda na Tanganyika na baadaye
Tanzania katika miaka kabla na baada ya uhuru wa nchi hizi.
Baada
ya kuvunjika kwa jumuiya ya Africa Mashariki, Shirika jipya la Reli (Tanzania
Railways Corporation) liliundwa kama Shirika la Umma. Shirika la Reli Tanzania
liliendelea kubeba jukumu zima la usafirishaji nchini Tanzania hivyo kuendelea
kutoa huduma za usafiri kwa njia ya reli (Reli Transport Services), majini
(Marine transport service), Barabara (Road transport service) na huduma za
Mahoteli na Migahawa (Hotels and Catering services). Shughuli za usafirishaji
nchini Tanzania ziliendelea kwa kutumia nyenzo zilizokuwepo, kwa sababu vifaa
vingi vilizuiliwa Nairobi –Kenya, ambako ndiyo yalikuwa makao makuu ya Jumuiya
na pia makao makuu ya Shirika la Reli la Afrika Mashariki.
Ubinafsishaji wa Shirika la Reli Tanzania
Kutokana
na ukweli kuwa, juhudi za kulifanya Shirika lijiendeshe kwa faida hasa baada ya
mipango ya ERP na RRP kutofikia viwango vilivyotarajiwa mwishoni mwa miaka ya
1990 wafadhili waliamua kusitisha kuendelea kuwekeza katika usafiri wa reli na
wakasisitiza sera ya ubinafsishaji.
Malengo
ya Kubinafsisha usafiri wa Reli yalikuwa,
- Kushirikisha wawekezaji kutoka sekta binafsi
- Kushirikisha menejimenti kutoka sekta binafsi
- Kuipunguza serikali mzigo wa shirika kutegemea bajeti ya serikali
- Kuingiza teknolojia za kisasa katika utendaji
Mnamo
mwaka 1998 Serikali iliidhinisha mpango wa ubinafsishaji wa Shirika la Reli
Tanzania uliotarajiwa kuanza April, 1998 na kumalizika Aprili 2000. Baada ya
mchakato mrefu, tarehe 6 Machi 2006 kampuni ya RITES ya India ilipewa taarifa
ya ushindi na baada ya taratibu zote kutimizwa ikiwemo kuanzishwa kwa Kampuni
ya Reli Tanzania (TRL) na Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli (RAHCO), uongoozi
wa RITES ulikabidhiwa uendeshaji wa huduma za usafiri wa Reli ya Tanzania kwa
kipindi cha miaka Ishirini na tano kuanzia Octoba 1, 2007. RITES ya India
ilikuwa na 51% ya hisa zote na Serikali ya Tanzania ilikuwa na 49%.
Hata
hivyo malengo yaliyotarajiwa kupatikana baada ya ubinafsishaji yalidhihirika
kutofikiwa, Serikali ya Tanzania iliamua kusitisha mkataba wa ukodishwaji mnamo
mwaka 2010 na kuanzia tarehe 22 Julai 2011 kampuni ilirudi mikononi mwa
serikali kwa umiliki wa asilimia mia moja(100%).
Kuundwa upya kwa Shirika la Reli Tanzania(TRC)
Mnamo
mwaka 2017 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipendekeza muswada wa
kufanyiwa marekebisho Sheria ya Reli Tanzania na kutungwa Sheria mpya ya Reli
ili kufuta iliyokuwa Kampuni ya Reli Tanzania(TRL) na Kampuni ya Rasilimali za
Reli(RAHCO) na hatimaye kuundwa kwa Shirika la Reli Tanzania(TRC) chini ya
Sheria mpya ya Reli Tanzania.