RAIS MAGUFULI AWEKA JIWE LA MSINGI UJENZI WA SGR AWAMU YA PILI - TRC Blog

Home Top Ad

"TOGETHER WE MOVE"

Thursday, March 15, 2018

RAIS MAGUFULI AWEKA JIWE LA MSINGI UJENZI WA SGR AWAMU YA PILI



Rais Dk.John Magufuli leo ameweka jiwe la Msingi la Ujenzi wa awamu ya pili ya Reli ya Treni ya Umeme kutoka Morogoro-Dodoma-Makutupora katika eneo la Ihumwa, Manispaa ya Dodoma kwa kumtaka Mkandarasi Yapi Merzeki kutoka Uturuki kukamilisha ujenzi wa Reli hii ndani ya muda ili Watanzania waanze kuona manufaa ya Reli hii ambayo itasaidia katika kukuza Uchumi wa Nchi na kurahisisha sekta ya Usafirishaji nchini Tanzania.

Reli hiyo itakuwa na uwezo wa kubeba tani 10,000 ambazo ni sawa na malori 500 yenye tani 20 kila moja ukilinganisha na reli ya zamani(metre gauge) ambayo hata ikifanyiwa maboresho haiwezi kufikia kiwango hiko, reli hiyo itasaidia kukuza uchumi wa nchi, kupunguza uharibifu wa mazingira, kusafirisha abira na mizigo na abiria kwa unafuu, uharaka na usalama lakini pia itaokoa barabara zetu kutokana na uharibifu unaotokana na mizigo mikubwa inayobebwa na malori.        

Rais Magufuli ameongeza kuwa Reli hii yenye gharama ya zaidi ya Tsh Trilioni 4 inajengwa kwa fedha za walipa kodi bila kupata ufadhili wowote na hivyo kutoa rai kwa Watanzania kulipa Kodi ili itumike kwa ajili ya kujiletea maendeleo katika nyanja mbalimbali. Wakati huo huo Rais Magufuli ameahidi ujenzi wa barabara ya lami kutoka barabara kuu ya Dar es salaam kuingia ndani eneo la Ihumwa.       

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akikata utepe kuashiria uwekaji wa jiwe la msingi ujenzi wa mradi wa Reli ya Kisasa itakayotumia umeme Standard Gauge (SGR) itakayotoka mkoani Morogoro hadi Makutupora Dodoma katika eneo la Stesheni ya Ihumwa nje kidogo ya mji wa Dodoma. Wengine katika picha ni Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa pamoja na Balozi wa Uingereza hapa nchini Sarah Cooke wakishuhudia.
Akimkaribisha Rais, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa amemuhakikishia Mh Rais kwamba atasimamia Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi CCM ili kuwaletea Watanzania maendeleo katika nyanja mbalimbali na kuwataka Watanzania kuchangamkia fursa zitakazotokana na ujenzi wa Reli hii ya Kati.   

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof Makame Mbarawa na Mkurugenzi wa TRC Ndg Massanja Kadogosa,kwa nyakati tofauti,wameelezea mradi huu wa Reli kama kati ya miradi michache inayotekelezwa Afrika na hivyo kuiweka Tanzania katika nchi zilizopiga hatua kubwa katika sekta ya Usafirishaji.  


Naye Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Mh Anthony Mavunde amempongeza Mh Rais Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya ya maendeleo ambayo yanaigusa Dodoma kwa kiwango kikubwa na kuwataka wanaDodoma wachangamkie fursa za ujenzi wa Reli na maendeleo makubwa yanayotokana na Dodoma kuwa makao makuu ya nchi.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akifunua kitambaa wakati akiweka jiwe la msingi ujenzi wa mradi wa Reli ya Kisasa itakayotumia umeme Standard Gauge (SGR) itakayotoka mkoani Morogoro hadi Makutupora Dodoma katika eneo la Stesheni ya Ihumwa nje kidogo ya mji wa Dodoma.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akifunga kifuniko mara baada ya kutumbukiza karatasi ya majina ya viongozi mbalimbali waliofanikisha ujenzi huo kama kumbukumbu katika uwekaji wa jiwe la msingi la Reli ya Kisasa(SGR) itakayotoka mkoani Morogoro-hadi Makutupora Dodoma.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiweka saruji iliyochanganywa na kokoto kwenye jiwe hilo la msingi la ujenzi wa Reli ya Kisasa mkoani Morogoro-hadi Makutupora Dodoma yenye urefu wa km 426 ukijumuisha na njia za kupishana katika eneo la Ihumwa stesheni mkoani Dodoma.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akikata utepe pamoja Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuashiria uzinduzi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa ya umeme kutoka mkoani Morogoro-hadi Makutupora Dodoma yenye urefu wa km 426 ukijumuisha na njia za kupishana katika eneo la Ihumwa stesheni mkoani Dodoma. Wengine katika picha ni Naibu Spika Dkt. Tulia Ackson, Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa,  Mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Reli TRC Masanja Kadogosa pamoja na viongozi wengine.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akikagua mfano wa Reli hiyo ya Kisasa itakayotumia umeme mara baada ya kuweka jiwe la msingi katika eneo la Ihumwa stesheni mkoani Dodoma.
Treni ya zamani ikipita katika Reli za zamani katika eneo la Ihumwa stesheni mkoani Dodoma.
Mtendaji Mkuu wa Shirika la Reli TRC Masanja Kadogosa akitoa maelezo ya mradi huo wa Reli ya kisasa ya umeme kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli
Sehemu ya wananchi mbalimbali waliohudhuria sherehe hizo za uwekaji wa jiwe la msingi.
Muonekano wa moja ya vituo vya treni vitakavyojengwa kwenye mradi huo wa SGR kutoka Morogoro hadi Makutupora

Muonekano wa moja ya mahandaki ya njia za treni yatakayojengwa kwenye mradi wa awamu ya pili ya SGR kutoka Morogoro hadi Dar es Salaam

Muonekano wa daraja la juu la treni ya umeme 

No comments:

Post a Comment